Gor Mahia waaga mashindano ya CECAFA Kagame

July 12, 2018

Hali sio hali katika kambi ya klabu ya Gor Mahia baada ya kubanduliwa nje ya mchuano wa CECAFA Kagame.

Gor Mahia walitandikwa mbao 2-0 na Azam katika nusu fainali iliyochezwa katika uga wa kitaifa jijini Dar es Salaam.

Mechi hiyo iliisha sare ya kutofungana katika muda wa kawaida na kupelekea kipindi cha muda wa nyongeza.

Ditram Nchimbi alianza kuifungia Azam kunako dakika ya 92 kabla ya Bruce Kangwa kuongeza la pili katika dakika ya 100.

Hii ni mara ya pili Kogallo wanapoteza kwa Azam. Mwaka 2015 walitandikwa mbao 2-0 katika fainali ya makala ya shindano hilo. K’Ogalo hawajashinda taji hili kwa muda wa miaka 33.

Mara ya mwisho Gor Mahia walishinda taji hili ilikuwa ni mwaka wa 1985 walipowashinda mahasimu wao AFC Leopards 2-0 wakati shindano hilo lilipofanyika nchini Sudan.

Tusker FC ndio klabu ya mwisho kutoka Kenya kuwahi kushinda taji hilo ikiwa ni mwaka 2008 walipoifunga Uganda Revenue Authority 2-1 nchini Tanzania.

Taarifa na Dominick Mwambui.

RADIO KAYA 93.1 FM (MSA), 99.7 FM (MLD) NA 94.9 VOI NA VIUNGA VYAKE.