Harambee Stars yapanda nafasi tano

September 20, 2018

Kenya-vs-Ghana-AFCON-3

Timu ya taifa ya soka ya wanaume Harambee Stars imepanda nafasi tano katika viwango vya soka kulingana na FIFA.

Katika orodha hiyo mpya timu ya taifa ya Ubelgiji na Ufaransa kwa mara ya kwanza katika historia zinashikilia nambari moja ulimwenguni.

Kuimarika huku kwa Kenya kunajiri baada ya kuandikisha ushindi wa 1-0 dhidi ya Ghana kwenye mechi iliyochezwa Septemba 8 katika uga wa Kasarani. Kenya sasa inaratibiwa ya 107.

Wapinzani wa Kenya katika mbio za kufuzu kwa kombe la mataifa ya bara Afrika 2019 ( AFCON 2019) Ethiopia wameimarika kwa kupanda nafasi mbili kutoka 151. Ethiopia waliishinda Sierra Leone 1-0.

Uganda bado inaongoza ukanda wa Afrika Mashariki licha ya kuporomoka nafasi moja hadi 83. Sudan ni ya tatu ikiwa imeratibiwa ya 132.

Barani Afrika Tunisia inaongoza ikishikilia nafasi ya 23 baada ya kupanda nafasi moja. Senegali ni ya pili ikiwa imeratibiwa ya 25 huku Congo DRC ikifunga tatu bora ikiwa imeratibiwa ya 40.

Taarifa na Dominick Mwambui.

 

RADIO KAYA 93.1 FM (MSA), 99.7 FM (MLD) NA 94.9 VOI NA VIUNGA VYAKE.