Mahakama kuu ya Malindi yaagiza kuzuliwa kwa korokoroni maafisa wawili wa polisi wanaokabiliwa na kesi ya mauji

February 12, 2019

Mahakama kuu ya Malindi imeagiza kuzuliwa kwa siku mbili katika kituo cha polisi cha Malindi, maafisa wawili wa polisi wanaokabiliwa na kosa la mauaji ili wafanyiwe uchunguzi wa kiakili.

Agizo hilo limetolewa na Jaji Weldon Korir, baada ya Kiongozi wa mashtaka katika Mahakama hiyo Babra Zombo kuiomba mahakama kumpa mda huo ili washukiwa hao wafanyiwe uchunguzi katika hospitali kuu ya Malindi kabla ya kuanza kujibu mashtaka yanayowakabili.

Washukiwa hao ni pamoja na Simeon Oyoo Ayodo pamoja na mwenzake Amos Kiptoo Kipsang kutoka kituo cha polisi cha Mariakani kaunti ya Kilifi, wanaodaiwa kumpiga risasi na kumuua Katana Kazungu katika hali tatanishi eneo la Kaloleni mnamo tarehe 26, mwezi Juni mwaka 2018.

Wakili wa washukiwa hao Matete Katoto ameiomba Mahakama iwaachilie kwa dhamama wateja wake, ombi ambalo Jaji Korir amelikataa, akisema washukiwa hao bado hawajasomea mashtaka.

Jaji Korir ameahirisha kesi hiyo hadi Alhamisi tarehe 14 mwezi Februari mwaka huu ambapo kesi hiyo itaanza kusikizwa.

Taarifa na Charo Banda.

RADIO KAYA 93.1 FM (MSA), 99.7 FM (MLD) NA 94.9 VOI NA VIUNGA VYAKE.