Mbunge wa Jomvu aamrisha kukamatwa kwa wanaokata mikoko

February 8, 2019

Mbunge wa Jomvu Badi Twalib awataka maafisa wa Mamlaka ya Mazingira nchini NEMA na wale wa misitu, kuwakamata watu wanaoendeleza tabia ya uharibifu wa mikoko katika eneo la Jomvu.

Akizungumza na Wanahabari, Badi amesema visa vya ukataji wa mikoko katika eneo hilo vimekithiri mno na kupelekea kushuhudiwa kwa asilimia 20 pekee ya mikoko katika eneo hilo.

Amesema kama mbunge wa eneo hilo hatokubali kushuhudia baadhi ya watu wakiharibu Mazingara ya eneo bunge hilo, akisema ni lazima hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya watu kama hao.

Badi ameongeza kuwa uharibifu huo umesababisha madhara makubwa katika sekta ya uvuvi, akisema viwango vya uvuvi katika eneo hilo vimedorora kwa kiasi kikubwa.

Wakati uo huo amewataka wakaazi wa eneo hilo kuwa mstari wa mbele kulinda Mazingira ya baharini kwa kupanda miche ya mikoko huku akiwahimiza kujitenga na biashara ya ukataji miti.

Taarifa na Hussein Mdune.

RADIO KAYA 93.1 FM (MSA), 99.7 FM (MLD) NA 94.9 VOI NA VIUNGA VYAKE.