Meneja wa klabu ya Bandari aaga dunia

January 4, 2018

Meneja wa klabu ya Bandari Alfred Obwaka ameaga dunia.

Kulingana na taarifa iliyotundikwa katika mtando wa kijamii wa klabu hiyo, Obwaka ameaga dunia usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya MEWA mjini Mombasa.

Inasemekana kuwa Obwaka alizimia bafuni nyumbani kwake eneo la Majengo muda mfupi baada ya kutizama mechi kati ya Arsenal na Chelsea. Alikimbizwa katika hospitali ya Al Farooq lakini alielekezwa katika hopitali ya MEWA kutokana na ukosefu wa hewa ya Oxygen. Ni katika hospitali ya MEWA alipotangazwa kuwa amefariki muda mfupi baada ya kuwasili.

Obwaka aliisaidia Bandari kushinda taji la Ngao ya GO TV mwka 2015 na mashindano ya KECOSO mwaka wa 2016 na 2017.

Alianza usakataji soka miaka ya 90 katika klabu ya Lake Warriors kabla ya kujiunga na Coast Stima ambapo alikuwa nahodha msaidizi na kuisaidia kunyakua taji la dhahabu la Moi mwaka wa 1999 uwanjani Kasarani dhidi ya Mumias Sugar. Baadaye alijiunga na Bandari FC ambapo alihudumu kama naibu mkufunzi mchezaji kati ya mwaka wa 2003 na 2004 kabla ya kuwa meneja mwaka wa 2005.

Taarifa na Dominick Mwambui.

RADIO KAYA 93.1 FM (MSA), 99.7 FM (MLD) NA 94.9 VOI NA VIUNGA VYAKE.