Mwakwere kutafuta haki katika Mahakama ya Upeo

May 17, 2018

Mahakama ya Rufaa mjini Mombasa imelitupilia mbali ombi la kuwajumuisha walalamishi wengine 3 kwenye kesi ya kupinga uchaguzi wa Gavana wa Kwale Salim Mvurya.

Akitoa uamuzi huo, Jaji wa Mahakama ya Rufaa mjini Mombasa Wanjiru Karanja amesema uamuzi huo umeafikiwa na jopo la majaji watatu waliokuwa wakisikliliza kesi hiyo.

Jaji Karanja amesema jopo hilo limebaini kuwa mlalamishi wa kwanza Mwalole Tchappu Mbwana alikuwa tayari ameiondoa kesi hiyo Mahakamani licha ya ombi hilo lililowasilishwa mwezi uliopita na jopo la mawakili watatu wa mlalamishi kudaiwa kutozingatia vigezo hitajika na sheria za uchaguzi.

Akizungumzia swala hilo nje ya majengo ya Mahakama hiyo, aliyekuwa mgombea wa kiti cha ugavana kaunti ya Kwale kwa tiketi ya chama cha Wiper wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, Balozi Chirau Ali Mwakwere ameeleza kutoridhishwa na uamuzi huo, huku akisema ataelekea katika Mahakama ya upeo kutafuta haki.

Taarifa na Hussein Mdune.

RADIO KAYA 93.1 FM (MSA), 99.7 FM (MLD) NA 94.9 VOI NA VIUNGA VYAKE.