Safari ya “chungu” cha wamijikenda yaanza upya

February 4, 2019

Safari ya chungu cha wamijikenda imeanza upya.

Safari hiyo imeanzisha upya na Radio Kaya katika harakati za kukifundisha kizazi kipya utamaduni wa jamii hiyo.

Hatua hii ni ukumbusho wa safari iliyopigwa na wamijikenda kutoka Shungwaya hadi katika maeneo wanamoishi sasa.

Kupitia kwa kipindi Malenga wa Kaya kinachoendeshwa na Bahati Ngazi na Nassir Maulid, Radio Kaya inalenga kukifundisha kizazi cha sasa kuhusiana na utamaduni wa Wamijikenda.

“Katika safari hii tutakuwa tunatembelea kila eneo ili kufahamu utamaduni wa sehemu hiyo. Kupitia kwa mashairi msiklizaji ataweza kuchangia kando na kuuliza maswali hewani,” amesema Bahati.

Mtangazaji huyo ameongeza kuwa jamii ya Waswahili pia itajumuishwa kwenye chungu.

“Tumeona ni vyema pia tujumuishe jamii ya waswahili katika chungu kwani lugha ya kiswahili imekuwa na sehemu kubwa katika jamii ya mpwani, hivyo basi mswahili ni mmoja wetu,” amesema Bahati.

Katika historia inaaminika kuwa wamijikenda walikuwa na chungu maalum ambacho walikichunga sana katika safari yao kutoka Shungwaya. Chungu hicho kinasemakana kuwa kilivunjika walipofika katika eneo linaloitwa Digo. Kuvunjika kwa chungu hicho ndiko  ambako kulipelekea jamii inayoishi sehemu hiyo kuitwa wadigo.

Neno Digo ni mchanganyiko wa vitendo viwili “Di” yaani kuanguka na “Go” kumalizika kwa chungu.

Taarifa na Dominick Mwambui.

RADIO KAYA 93.1 FM (MSA), 99.7 FM (MLD) NA 94.9 VOI NA VIUNGA VYAKE.