Shule ya Galana yafungwa kwa muda usiojulikana

July 10, 2018

Idara ya Elimu kule Magarini kaunti ya Kilifi imeifunga shule ya upili ya Galana kwa mda usiojulikana baada ya wanafunzi kugoma mapema leo.

Akithibitisha kufungwa kwa shule hiyo, Katibu wa chama cha KNUT tawi la Malindi na Magarini Fredrick Nguma amesema wanafunzi hao waliingiwa na uoga baada ya mwanafunzi mmoja wa kidato cha nne kuugua na kisha kufariki katika mazingira tatanishi.

Kulingana na Nguma, uamuzi huo umeafikiwa na bodi ya shule hiyo kufuatia visa vya kushtua kushuhudiwa shuleni humo na kuwatia wasiwasi wanafunzi.

Aidha amesema hatua hiyo pia itazuia uharibifu kutokea shuleni humo huku akihoji kuwa bodi ya shule hiyo itawasiliana na wazazi na wanafunzi hao kuhusu tarehe rasmi ya wanafunzi kurejea shuleni.

Taarifa na Charo Banda.

RADIO KAYA 93.1 FM (MSA), 99.7 FM (MLD) NA 94.9 VOI NA VIUNGA VYAKE.