Wamiliki wa matatu wampongeza Rais kwa kuiondoa NTSA barabarani

January 11, 2018

MBARACK-3

Chama cha wamiliki wa matatu kanda ya Pwani kimeipongeza hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kuamrisha kuondoka barabarani maafisa wa mamlaka ya uchukuzi na usalama barabarai NTSA.

Kupitia Mshirikishi wake Salim Mbarack chama hicho kimeitaja hatua hiyo kama mwafaka zaidi kwani mara nyingi maafisa wa NTSA wamekuwa wakihitilafiana na utendakazi wa maafisa wa trafiki.

Akizungumza na radiokaya Mbarack amesema kwamba hatua hiyo itatoa fursa kwa NTSA kubuni sera mahsusi za kuiboresha zaidi sekta ya uchukuzi nchini na kufanikisha utekelezaji wa sera hizo kupitia kwa maafisa wa trafiki.

Mbarack aidha ameihimiza NTSA kubuni sera mwafaka kukabili kikamilifu changamoto za uchukuzi ikiwemo ajali za mara kwa mara kwenye bara bara kuu za humu nchini.

Kauli ya mshirikishi huyo wa chama cha wamiliki wa matatu kanda ya Pwani inajiri baadaya rais Kenyatta kuwaamrisha maafisa wa mamlaka ya uchukuzi na usalama barabarani kuondoka barabarani na kuwaacha maafisa wa trafiki kutekeleza majukumu yao bila muingilio.

Taarifa na Cyrus Ngonyo.

RADIO KAYA 93.1 FM (MSA), 99.7 FM (MLD) NA 94.9 VOI NA VIUNGA VYAKE.