Wananchi Kilifi walalamikia kupuuzwa kwa mapendekezo yao kuhusu bajeti

June 5, 2018

Huku kamati ya bajeti ya bunge la kaunti ya Kilifi ikikamilisha vikao vyake vya kukusanya maoni ya wananchi wa kaunti hiyo, wananchi wameishtumu kamati hiyo kwa kupuuza maoni yao kila wanapotoa mapendekezo.

Wakiongozwa na Mvera Kazungu wananchi hao wamesema kwamba bajeti hiyo haijaipa kipaumbele miradi ya kunufaisha mwananchi wa chini huku wakishtumu mradi wa ujenzi wa nyumba ya naibu gavana ambao umetengewa kima cha shilingi milioni 214.

Wakitoa maoni yao, wameitaka kamati hiyo kupunguza kiasi hicho hadi shilingi milioni ishirini ili fedha zengine zitumike kwa miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya bajeti ya bunge la kaunti ya Kilifi Albert Kiraga ameahidi wananchi hao kuwa kamati hiyo itahakikisha maoni ya mwananchi yanaheshimiwa.

Hata hivyo Kiraga ambaye pia ni mwakilishi wa wadi ya Gongoni amewanyoshea kidole cha lawama mawaziri na maafisa wakuu katika kaunti hiyo kwa kutowahamasisha wananchi kuhusu masuala muhimu yanayoihusu kaunti.

Taarifa na Marrieta Anzazi.

RADIO KAYA 93.1 FM (MSA), 99.7 FM (MLD) NA 94.9 VOI NA VIUNGA VYAKE.