Wizara ya elimu yahimizwa kujumuisha elimu ya ngono kwenye mtaala

May 7, 2018

Wizara ya elimu imehimizwa kujumuisha elimu kuhusu maswala ya ngono na ushauri shuleni ili kuwawezesha Wanafunzi kupewa mwelekeo unaostahili katika umri mdogo.

Mkurugenzi wa Shirika la Vijana la ‘Stretchers Youth Organization’ Dickson Okong’o amesema kwamba kinyume na siku za hapo awali ambapo watoto walikuwa na ufahamu mchache mno kuhusu mambo ya ngono na maswala mengine ya kimaisha, kwa sasa watoto wana ufahamu wa kina kuhusiana na maswala hayo.

Akizungumza huko Changamwe Kaunti ya Mombasa Okong’o amesema kwamba kupitia kwa maswala ya utandawazi na watoto kuwa na ufahamu zaidi kuhusiana na mambo ya teknolojia, sasa watoto hao wanashiriki ngono bila ya kujali maambukizi ya maradhi au uja uzito.

Okong’o ameitaka Wizara ya elimu kuwaruhusu washauri wa Vijana kuzuru shuleni angalau mara moja kwa juma ili kukaa na Wanafunzi na kujadili kuhusu maswala ya ngono na pia kuwaelekeza vyema maishani ili wasipotoke kimaadili au kukatiza ndoto zao maishani.

Taarifa na Gabriel Mwaganjoni.

RADIO KAYA 93.1 FM (MSA), 99.7 FM (MLD) NA 94.9 VOI NA VIUNGA VYAKE.