Baraza la mawaziri nchini limeidhinisha sera ya kitaifa kuhusu jamii za wachache, jamii zilizotengwa na wenyeji asili, na kupitishwa sera hiyo kutahakikisha mageuzi katika mchakato wa uajiri kwenye huduma za umma.
Rais William Ruto wakati akitoa tangazo hilo amesema sera hiyo itahakikisha jamii za wachache zinajumuishwa na kuwakilishwa kikamilifu katika taasisi zote za serikali kuambatana na katiba ya nchi.
Akizungumza katika ikulu ya Nairobi wakati wa hafla ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wachache, rais Ruto amesema kuidhinishwa sera hiyo ni hatua kubwa katika kukabili ukosefu wa usawa uliodumu kwa muda mrefu katika huduma za umma.
Kiongozi wa taifa aidha ameagiza idara ya ulinzi wa jamii, kusajili mara moja familia kutoka jamii za wachache zilizotimiza vigezo, katika miradi ya serikali ya kukimu wasiojiweza ikiwemo mradi wa Inua jamii.



