Monday, 19January, 2026    7:36 am

Play Listen Live

Chama cha UDA kimetoa ratiba ya uchaguzi wa mashinani wa chama hicho.

Chama cha UDA leo Disemba 4, kimefungua rasmi usajili wa wagombea wanaotaka kushiriki uchaguzi wa viongozi wa mashinani wa chama hicho.

Bodi ya uchaguzi ya chama cha UDA kwenye taarifa yake leo Alhamisi, imesema usajili huo unaofanyika kwenye tovuti ya chama hicho, utakamilika rasmi tarehe 23 mwezi huu wa Disemba.

Akitoa tangazo hilo mwenyekiti wa bodi hiyo Anthony Mwaura amesema kuanza zoezi hilo la kusajili wagombea, kunatoa nafasi ya kuandaliwa uchaguzi katika kaunti 20 zilizosalia.

Uchaguzi huo wa viongozi wa mashinani wa chama cha UDA umeratibiwa kufanyika tarehe 10 mwezi Januari mwaka 2026, katika kaunti za Baringo, Bomet, Elgeyo Marakwet, Kericho, Nakuru, Nandi, Trans Nzoia, Uasin Gishu, Samburu, Embu, Kiambu, Kirinyaga, Laikipia, Meru, Murang’a, Nyandarua, Nyeri, Tharaka-Nithi, Kakamega, na Vihiga.

Uamuzi wa kuanza usajili huo umeafikiwa baada ya kikao cha pamoja kati ya kamati kuu ya uongozi wa chama cha UDA na bodi ya uchaguzi ya chama hicho, kikao kilichoongozwa na naibu rais Prof Kithure Kindiki.

Wakati hayo yakijiri, chama hicho cha UDA kimepata pigo baada ya wapiga kura wawili kuwasilisha kesi mahakamani, kupinga ushindi wa  mgombea wa chama hicho aliyeshinda uchaguzi mdogo wa ubunge wa Mbeere-Kaskazini Leonard Wamuthende.

Wawili hao wamewasilisha kesi hiyo leo , wakitaka kubatilishwa ushindi wa Wamuthende na kuandaliwa uchaguzi mpya.

Story by Mimuh Mohamed

Contact Details

Radio Kaya

P.O Box 172~80403
Kwale, Kenya

SMS  – 0702 885 885

General Enquiries
info@radiokaya.co.ke

© 2025 Radio Kaya. All rights reserved.