Licha ya Serikali kuitambua rasmi jinsia ya tatu humu nchini yaani watu waliyo na maumbile tata au Huntha, jamii hiyo imekuwa ikibaguliwa mashinani.
Afisa kutoka Shirika linaloangazia haki za watu wasiyokuwa na jinsia moja rasmi yaani Huntha la Intersex Rights Initiative Coast-IRIC, Amina Ningala amesema ni vyema kwa jamii mashinani kuwakubali watu hao na kuwawezesha kujitambua kadri wanavyokuwa kwani kuwabagua kimaumbile ni kuwanyanyasa na kuwasababishia changamoto za kisaikolojia maishani.
Akizungumza katika kaunti ya Mombasa, Bi Ningala amesema mara nyingi wazazi wa watu hao waliyo na jinsia tata wamehofia kejeli za jamii hali inayopelekea Huntha kufanyiwa upasuaji ambao baadaye humuathiri mtoto hata zaidi kimaumbile na kisaikolojia vile vile.
Mtetezi huyo wa haki za watu waliyo na jinsia tata Pwani yaani Huntha amekariri kwamba mara nyingi akina mama katika ndoa wamehangaishwa na kukejeliwa kwa kudaiwa kuchangia hali hiyo, hali ambayo imechangia dhuluma dhidi ya mwanamke na hata kuvunjika kwa ndoa, Ningala akisisitiza pindi mtoto anapozaliwa na utata wa kijinsia anapaswa kupata usaidizi na malezi ya wazazi wote wawili.
Story by Gabriel Mwambeyu



