Huku ulimwengu ukiadhimisha siku ya ukwimwi duniani leo Disemba Mosi, shirika la afya duniani WHO limesema kumaliza maambukizi ya HIV kufikia mwaka 2030, kunahitaji mikakati inayoangazia zaidi haki za kibinadamu, ushirikiano wa kimataifa, na uongozi wa kisiasa endelevu.
WHO imesema licha ya mafanikio kushuhudiwa katika mapambano dhidi ya HIV kwa miongo kadhaa sasa, makabiliano hayo yako katika njia panda, wakati huu ambapo huduma za kuokoa maisha zinatatizwa, huku jamii zikiwa kwenye hatari.
Shirika hilo kwenye ripoti yake limeeleza kwamba kufikia mwaka uliopita wa 2024, watu milioni 40.8 walikua wanaishi na maambukizi ya virusi vya ukimwi duniani.
Shirika hilo vile vile limesema mwaka huo wa 2024, watu laki 6 na elfu 300 walifariki kutokana na virusi vya ukimwi huku maamukizi mapya milioni 1.3 yakinakiliwa.
Wizara ya afya humu nchini imesema imejikita kumaliza HIV kufikia mwaka 2030, ikiwemo kukabili vitisho vitatu vinavyoathiri vijana wanaobaleghe na vijana wadogo, ikiwemo maambukizi ya HIV, mimba za utotoni na dhulma za kingoni na kijinsia.
Katibu katika wizara ya afya nchini Dkt Mary Muthoni amesema watu milioni 1.3 humu nchini Kenya wanaendelea na matibabu ya HIV, na maambukizi mapya yamepungua kwa asilimia 72, vifo vinavyotokana na HIV vimepungua kwa asilimia 90 na maambukizi ya HIV kutoka kwa mama hadi kwa mtoto yamepungua kwa asilimia 35.
Story by Mimuh Mohamed



