Licha ya watetezi wa haki za kibinadamu nchini kupigania haki na kuishinikiza Serikali kuheshimu haki za wananchi, Serikali imeendeleza ukiukaji mkubwa wa haki za Wakenya bila kujali.
Afisa wa maswala ya dharura wa Shirika la kutetea haki za kibinadamu nchini la MUHURI Francis Auma amesema Kenya inashuhudia ukiukaji mkubwa mno wa haki za kibinadamu unaostahili juhudi za Wakenya wote ili kuidhibiti hali hiyo.
Akizungumza katika Kaunti ya Mombasa hii leo, Auma amevikosoa zaidi vitengo mbalimbali vya Serikali ikiwemo Idara ya mahakama kwa kushindwa kupigania haki kwa mwananchi, huku vitengo vya usalama vikikiuka haki za wananchi kwa kuwatia nguvuni kiholela na kuwapoteza baadhi ya Wakenya hasa katika Ukanda wa Pwani na Kaskazini Mashariki.
Wakati uo huo, Mtetezi huyo wa haki za kibinadamu nchini amedhihirisha hofu yake kufuatia ukukaji mkubwa wa haki za kibinadamu hasa katika Jumuiya ya Afrika mashariki, akiulaumu muungano wa mataifa ya Bara la Afrika AU kwa kusalia kimya huku Viongzi wa mataifa ya Tanzania, Uganda na Kenya wakiendeleza unyama dhidi ya wananchi wake.
Kauli ya Auma inajiri baada ya hapo jana Kenya kujiunga na ulimwengu katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya haki za kibinadamu, huku Mashirika yakilalamikia ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu nchini hususan mauaji ya kiholela yakiwemo yale yaliyokilenga kizazi cha Gen-Z kati ya mwezi Juni mwaka wa 2024 na Julai, 2025.
Story By Gabriel Mwambegu



