Huku maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani yakitarajiwa kuandaliwa kesho Disemba Mosi, katibu katika wizara ya afya Dkt Mary Muthoni amesema Kenya imepiga hatua katika mapambano dhidi ya HIV.
Akizungumza na wanahabari Dkt Muthoni amesema katika miongo miwili iliyopita maambukizi ya HIV pamoja na vifo vinavyotokana na maambukizi ya virusi vya ukimwi yamepungua kwa kiwango kikubwa.
Muthoni amesema maambukizi mapya ya HIV yamepungua kwa asilimia 72, vifo vinavyotokana na ukimwi vimepungua kwa asilimia 90 na maambukizi ya HIV kutoka kwa mama hadi kwa mtoto yakipungua kwa asilimia 35.
Dkt Muthoni aidha amesema kwa sasa zaidi ya wakenya milioni 1.3 wanaendelea na matibabu ya HIV, na kwamba serikali ya kitaifa imejikita kusongeza mbele mafanikio katika vita dhidi ya HIV.
Muthoni amewarai vijana wadogo kufanya maamuzi ya busara, kuepuka utumizi wa mihadarati, akionya kwamba tabia hizo zinawaweka kwenye hatari kupata maambukizi ya HIV na hatari nyengine za kiafya.
Sherehe za maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani zinaandaliwa katika kaunti 47 nchini, akisisitiza kwamba Kenya imejikita kumaliza HIV kama tishio la afya umma kufikia mwaka 2030.
Story by Mimuh Mohamed



