Kinara wa chama cha WIPER Kalonzo Musyoka ametangaza kwamba muungano wa upinzani utawasilisha kesi mahakamani, kupinga matokeo ya uchaguzi mdogo wa ubunge wa Mbeere-Kazini,kaunti ya Embu kwa misingi kwamba matokeo hayo yalikua na dosari.
Akizungumza leo Jumapili Kalonzo amepuuzilia mbali kauli kwamba chama tawala cha UDA kilishinda ubunge wa Mbeere-kaskazini na ubunge wa Malava, akisema chama hicho kinatambua wazi kwamba hakikushinda uchaguzi huo kihalali.
Kalonzo amedai kwamba kulikua na vitendo vya kuhitilafiana na kura za Mbeere kaskazini, akidai kwamba wana Ushahidi unaothibitisha kwamba watu wenye ushawishi walipiga simu wakati zoezi la kuhesabu kura likiendelea.
Kalonzo amesema wamekusanya ushahidi wa kutosha wa kudhibitisha madai hayo mahakamani.
Katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Mbeere Kaskazini, mgombea wa UDA Leonard Wamuthende aliibuka mshindi kwa kupata kura elfu 15,802 na kumpiku mpinzani wake wa karibu Newton Kariuki aliyepata kura elfu 15,308



