Story by Gabriel Mwaganjoni-
Mwanamke mmoja katika eneo la Chaani kaunti ya Mombasa anapigania uhai wake katika hospitali ya Portreiz eneo la Changamwe baada ya kuchomwa na mumewe usiku wa Jumatano.
Jeril Atieno wa umri wa miaka 22 amekuwa katika ndoa hiyo ya miezi mitatu na mumewe Joseph Kimondio wa umri wa miaka 25, ndoa ambayo imekumbwa na mzozo tangu mwanzoni.
Atieno ameeleza kwa masikitiko jinsi alivyohangaika kujiokoa kutokana na moto huo mkali.
Mamake Atieno, Jane Akoth anayemuuguza mwanawe katika hospitali hiyo ya Portreitz amesikitishwa na tendo hilo la kinyama, akisema ni lazima serikali ichukue hatua.
Akizungumza katika hospitali hiyo Daktari na mtaalam wa majeraha ya moto hospitalini humo Suhail Herman amesema Atieno amepata asilimia 25 ya majeraha ya moto na itamchukua muda wa takriban majuma mawili kuondoka hospitalini.
Tayari Kimondio ametiwa nguvuni na polisi na anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Chaani akisubiri kufikishwa Mahakamani.