Story by Gabriel Mwaganjoni –
Shughuli za kibiashara katika soko la Marikiti kaunti ya Mombasa zimetatizika pakubwa baada ya wakala mmoja anayekusanya kodi kutoka kwa wafanyabiashara sokoni humo kuwasili katika soko hilo na kukusanya mali ya wafanyabiashara hao.
Kulingana na Katibu wa Muungano wa wafanyabiashara hao Abdirahman Hussein mali ya zaidi ya shilingi milioni 2 imebebwa na wakala huyo aliyeandamana na Maafisa wa polisi.
Akiwahutubia Wanahabari sokoni humo, Hussein amesema hatua hiyo ni kinyume cha sheria kwani wakala huyo alikuwa na mgogoro na mfanyabiashara mmoja na wala sio zaidi ya wachuuzi 20 ambao wamepoteza mali yao.
Wakati uo huo, mmoja wa wafanyabiashara hao Mohamud Jaylani ametaka mzozo huo kutanzuliwa mara moja na wafanyabishara hao kupata mali yao yote.