Shirika la Search for Common Groud chini ya ufadhili wa European Union limewahimiza wakaazi wa kaunti ya Kwale kuzingatia kikamilifu masharti ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona.
Akizungumza na Wanahabari baada ya kutoa ufadhili wa vifaa vya kudhibiti Corona ikiwemo barakoa, viezi na mitungi ya maji kwa wananchi, maafisa wa usalama na wafanyibiashara, Afisa wa miradi katika shirika hilo Zena Hassan amesema hatua hiyo itadhibiti maambukizi.
Zena amesema kupitia mradi wa pamoja dhidi ya Corona, wanalenga kuwakidhi wakaazi walio katika athari zaidi ya kupata maambukizi hasa katika kaunti sita ikiwemo za Pwani na Nairobi.
Wakati uo huo ameweka wazi kwamba malengo ya shirika hilo ni kuhakikisha wananchi na maafisa wa usalama wanashirikiana katika kujanga uwiano wa kijamii ili kufanikisha vita dhidi ya Corona na kuimarisha usalama.
Kwa upande wake Kamishna wa kaunti ya Kwale Joseph Kanyiri amesema vifaa hivyo vitasaidia pakubwa kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona huku akiwahimiza wananchi kuhakikisha wanajikinga kikamilifu.