Tamasha la Mr and Ms Samba limeratibiwa kufika kilele siku ya jumamosi tarehe 20 Desemba katika ukumbi wa Aveon Schools huko Kinondo eneo bunge la Msambweni kaunti ya Kwale.
Mkurugenzi wa shirika la Samba Sports Youth Trust muandalizi mkuu wa tamasha hilo Mohammed Mwachausa, amesema tamasha hilo halijajikita katika masuala ya ulimbwende pekee bali pia katika masuala yanayowajenga vijana katika jamii.
Akizungumza katika ukumbi huo baada ya Mtanange wa Kirafiki baina ya timu ya Denmark FC na timu ya Rwafa kukaribisha kilele cha Tamasha hilo siku ya Jumatano, Mwachausa ameeleza kwamba vijana wanaoshindana katika tamasha hilo wataweza kuelezea miradi wanayolenga kutekeleza katika jamii.
Amesema miongoni mwa miradi ambayo itaangaziwa zaidi katika mashindano hayo ni pamoja na uboreshaji wa mazingira, afya ya uzazi, kupambana na mihadarati miongoni mwa miradi mingine.



