Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC imewataka wanasiasa kukoma kuwatisha maafisa wa tume hiyo wakati wa uchaguzi.
Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon amesema wameshuhudia tabia ya hatari ambapo wanasiasa wanaojiita mawakala wa wagombea fulani, kuingia kwenye vituo vya kupiga kura na kuvuruga mchakato wa upigaji kura.
Akizungumza jijini Nairobi wakati wa kikao cha wadau tofauti cha kutathmini uchaguzi mdogo ulioandaliwa Novemba 27, Ethekon amesema tume ya IEBC kamwe haitovumilia vitendo hivyo.
Ethekon amesema kushambulia maafisa wa IEBC ni uhalifu na wanaotekeleza uovu huo lazima wawajibishwe, akisema baadhi ya wanasiasa uingia kwenye vituo vya kupiga kura wakiwa wameandamana na makundi ya wafuasi wao na kuanza kuwaelekeza maafisa wa IEBC jinsi ya kutekeleza kazi zao.
Ethekon amesema iwapo tabia hiyo haitokomeshwa,huenda uaminifu wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 ukawa mashakani, kwani vitendo hivyo huenda vikaharibu mazingira ya uchaguzi huo.
Katika kikao hicho cha leo Jumatatu IEBC imewaalika wadau tofauti wakiwemo wanasiasa walioshiriki uchaguzi mdogo wa Novemba 27, wanahabari na taasisi za serikali kutathmini matukio yalioshuhudiwa wakati wa uchaguzi huo.
Story by Mimuh Mohamed



